Muhoozi aahidi kuimarisha jeshi la Uganda

0
363

Mtoto wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameahidi kupambana na ufisadi ndani ya jeshi baada ya kuchukua usukani kama kamanda mkuu wa juu wa jeshi hilo.

Museveni mwenye umri wa miaka 79, ambaye ameiongoza Uganda kwa miaka 38 alimtangaza mtoto wake, Muhoozi Kainerugaba, mwenye umri wa miaka 49 kuwa mkuu wa Jeshi la Uganda (UPDF) wiki iliyopita.

Katika hafla rasmi ya kukabidhiwa madaraka, Muhoozi ameapa kuimarisha ustawi wa wanajeshi kwa kupambana na tatizo la ufisadi pamoja na utawala mbaya wa rasilimali zilizopo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na jeshi.

Jeshi la Uganda linashikilia nafasi muhimu kieneo, wakati likiwa na vikosi vya kulinda amani kwenye mataifa ya Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambako vinakabiliana na makundi ya wanamgambo wa Kiislamu.

Upinzani nchini Uganda umemshutumu Museveni kwa kumpandisha cheo mwanawe katika jeshi ukidai anamuandaa kuchukua uongozi wa kisisasa, madai ambayo Museveni amekuwa akiyakanusha.