“Natarajia kuwakosa baadhi ya wachezaji wangu nyota. Siwezi kuhatarisha afya za wachezaji ambao bado hawana utimamu wa kimwili. Lakini kuna uwezekano mkubwa wa kukosa wachezaji watatu mpaka wanne,” amesema Kocha wa Yanga SC, Miguel Gamondi kuelekea mchezo dhidi ya Mamelodi Sundowns Machi 30 mwaka huu.
Amesema wachezaji ambao wako hatarini kukosa mchezo huo ni Kibwana Shomari, Khalid Aucho, Yao Kouassi na Pacôme Zouzoua kutokana na majeraha.
Aidha, amesema anatumaini kuwa Djigui Diarra na Aziz Ki ambao wamerejea leo watakuwa wapo salama na kwamba uamuzi wa mwisho kuhusu hatma ya wachezaji hao utajulikana leo katika mazoezi ya mwisho.
“Licha ya kukosa nyota wangu kwenye maandalizi, nina imani na wachezaji wengine ambao wapo kambini. Jambo muhimu ni kujitoa zaidi, kuliko Mamelodi. Sisemi kuwa hatuwafikii uwezo Mamelodi, ila naamini wana wachezaji wenye uzoefu mkubwa hivyo ni lazima vijana wangu wajitoe zaidi,” ameeleza Gamondi.