Muungano umekuwa chachu ya amani, maendeleo

0
320

Taarifa na Happyness Hans

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Suleiman Jafo amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umekuwa chachu katika kuleta amani, utulivu, mshikamano na maendeleo kutokana na ushirikiano mzuri uliopo baina ya pande mbili zinazounda muungano.

“Kuna nchi mbalimbali zimejaribu kuungana lakini bahati mbaya muungano huo haujaweza kudumu. Sisi Watanzania tumepata fursa hii na hasa tunapoelekea miaka 60 ya uhuru wetu, tunajivunia kwamba tumeweza kushikamana kwa utulivu na amani ya hali juu,” amesema Jafo leo Machi 26, 2024 wakati akizungumzia mafanikio miaka mitatu yaliyofikiwa na ofisi yake ndani ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan jijini Dodoma.

Amesema katika kipindi chote cha muungano, mambo takribani 22 ya muungano yameendelea kuwa muhimu na kuwa chachu ya maendeleo ya Watanzania.

Mbali na mafanikio ya kisiasa tangu kuungana kwa Zanzibar na Tanganyika na kisha vyama vya TANU na Afro Shirazi (ASP) mwaka 1977, amesema kumekuwa pia na mafanikio ya kijamii kupitia umoja wetu na kutengeneza misingi mizuri ya usalama.

Katika sekta ya elimu, amesema nchi imepata mafanikio makubwa kipindi chote cha muungano kwani shule za msingi zimeongezeka kutoka shule 3,200 kabla ya muungao hadi 20,562. Amesema sekondari mwaka 1961 zilikuwa 41 pekee lakini sasa zipo shule 6511.

Vivyo hivyo amesema pia katika sekta huduma nyigine zote kama afya, uchumi, umeme maji hadi miundombinu kumekuwa na maendeleo mkubwa ndani ya miaka mitatu ya uongozi wa Samia na miaka 60 ya uhuru.