Miradi ya maji inachangia kukuza uchumi

0
1320

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema serikali inawekeza katika Sekta ya Maji ili kukidhi mahitaji ya wananchi, hatua ambayo ina mchango katika kukuza uchumi.

Amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa Mapitio ya Sekta ya Maji 2024 jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Maji kitaifa 2024.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, Prof. Mkumbo amesema lengo kubwa la Serikali ni kukuza uchumi shindani na kuleta maendeleo ya watu na kwamba huduma ya maji ni moja ya jambo muhimu katika kufanikisha hatua hiyo nchini.

“Watendaji wa Sekta ya Maji wanafanya kazi kubwa na nzuri, tena usiku na mchana kwa ajili ya wananchi,” Prof. Kitila amesema na kuongeza kwamba Waziri wa Maji halali akipambania masuala ya maji kufika katika makazi ya wananchi.

Amesema hali ya upatikanaji wa maji imezidi kuongezeka mjini na vijijini na kwa kasi ilivyo, malengo yaliyowekwa na serikali ya CCM yatafikiwa ya asilimia 85 ya wanaopata maji salama vijijini na 95 mijini. Ameongeza kuwa takwimu za hali ya upatikanaji wa maji zinatokana na uwekezaji unaofanywa na serikali katika kufikisha huduma ya maji kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF) Haji Nandule amekabidhi hundi ya shilingi milioni 800 kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bunda baada ya kuwa mamlaka ya kwanza kukidhi vigezo vya mkopo nafuu unaotolewa kwa ushirikiano na Benki ya Uwekezaji (TIB).

NWF inatoa fedha za utekelezaji wa miradi ya maji hapa nchini na imefungua dirisha la mikopo ya masharti nafuu kwa kushirikiana na Benki ya TIB, hatua ambayo inafanikisha huduma ya miradi ya maji kwa jamii kupitia mamlaka za maji.