Papa Francis hana nia ya kustaafu kama ambavyo imekuwa ikivumishwa na amepanga kusalia katika wadhifa huo maisha yake yote, kulingana na tawasifu yake mpya.
Papa mwenye umri wa miaka 87, amesema “hakuna hatari (yoyote ya kiafya)” ya yeye kulazimika kujiuzulu licha ya uvumi kuwa anaweza kujiuzulu kufuatia mlolongo wa matatizo ya kiafya ambayo amekuwa akipitia.
“Ninaamini huduma ya papa ni ya maisha. Kwa hivyo sioni sababu ya kuiacha,” amesema.
Mapema mwaka huu, Papa Francis aliahirisha kufanya mikutano kadhaa na kutoonekana hadharani kwa vipindi fulani kutokana na kuzorota kwa afya yake.
Amekuwa akisumbuliwa na mafua ya mara kwa mara, ana shida ya kutembea na amekuwa akionekana mara nyingi akitumia kiti mwendo.