Neema yashushwa vijiji vinavyozunguka Ruaha

0
269

Zaidi shilingi Bilioni mbili zimetolewa kwenye vijiji 16 kati ya 84 vinavyozunguka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ili kubadilisha tabia za kuvamia hifadhi pamoja na kuwafanya wanawake kuacha maisha ya utegemezi na kuwa wazalishaji mali.

Fedha hizo zimetolewa na Serikali kupitia Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) unaosimamiwa na wizara ya Maliasili na Utalii.

Ili kuondoa uvamizi wa jamii ndani ya hifadhi mradi wa REGROW umetoa zaidi ya shilingi Milioni 820 kwa vijiji vitano ambavyo ni Mauninga, Tungamalenga, Itinundu, Chinugulu na Kinyika kwa ajili ya kuanzisha miradi ya kibiashara huku zaidi ya shilingi Milioni 287 zikitolewa kama fedha mbegu kwenye vikundi vilivyoundwa na vijiji hivyo.

Mhifadhi Priscus Mrosso kutoka kitengo cha Mahusiano na Jamii cha Hifadhi ya Taifa ya Ruaha amesema mbali na fedha hizo mradi wa REGROW unaofadhiliwa na Benki ya Dunia pia umetoa zaidi ya shilingi Milioni 680 kuwafadhili masomo watoto 218 kutoka vijiji 16 kwenye vyuo vya chini, kati na vyuo vikuu.