Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema amempeleka Daniel Chongolo kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe kwa kuwa anajua Chongolo anaufahamu vizuri mkoa huo, hivyo akamtaka akausimamie ipasavyo.
Amesema Mkoa wa Songwe unaiunganisha Tanzania na Zambia kupitia mpaka wa Tunduma na kwamba yapo mambo mengi ya kiuchumi yanayotokea huko hususani uhalifu wa kiuchumi unaojumuisha ukwepaji kodi na kubadilisha fedha kwa njia isiyo halali.
Aidha, Rais Samia amemtaka Chongolo kwenda kusaidiana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma ili kuendelea kuongeza mapato na kwamba mapato yanayopatikana Tunduma yanaweza kuendesha Mkoa wa Songwe na kutoa mchango serikalini.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo Ikulu Dar es Salaam, leo Machi 13, kwenye hafla ya uapisho wa viongozi aliowateua hivi karibuni.
Mbali na Chongolo, viongozi wengine walioapishwa leo, Rais amewapa maelekezo mbalimbali kutegemea maeneo yao.