Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema kila mtoto ametokana na mzazi ambaye ni Baba na Mama na mtoto huyo anaweza kuwa na mlezi ambaye ni ndugu wa wazazi.
Amesema kutokana na ukweli huo hakuna jambo linalosababisha kuwepo kwa watoto wanaoitwa wa mtaani kwani hakuna mtaa unaozaa watoto.
Akizungumza katika Kongamano la Makuzi na Malezi ya Awali ya Mtoto Ukanda wa Afrika Mashariki linaloendelea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, Chalamila amesema ikiwa jamii itakubali kuwa wapo watoto wa mtaani ni kielelezo kuwa jamii imekwama mahali.
Chalamilia ameongeza kuwa msingi wa jambo lolote huanzia chini, hivyo malezi na makuzi ya mtoto yakifanyika katika msingi mzuri ni njia mojawapo ya kumkuza mtoto ili kuwekeza katika mtaji na hatimaye kuwa na Taifa lenye watu wazuri na wanaojiweza.