Rais Samia Suluhu Hassan amesema ataendelea kuwawezesha Watanzania ili ifikapo mwaka 2030 zaidi ya asilimia 88 wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
“Ahadi yangu kwenu ni kuhakikisha asilimia kubwa ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia na hili nitalivalia njuga, kuhusu masuala ya jinsia na watu walio kwenye makundi maalumu nitaendelea kusimamia kuhakikisha tunaondokana na changamoto zilizopo,” amesema.
Ameyasema hayo leo Jumapili Machi 10, 2023 alipozungumza kwa njia ya simu na wanawake waliojitokeza katika hafla ya kumpongeza kwa kuwa kinara wa nishati safi ya kupikia, mazingira na afya ya mama na mtoto iliyofanyika katika Ukimbu wa Diamond Jubelee, Dar es Salaam, ambapo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikuwa mgeni rasmi.
Kwa upande wake, Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kumuunga mkono Rais Samia ili aweze kutimiza maono yake ya kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, utunzaji wa mazingira pamoja na uimarishaji wa afya ya mama na mtoto kwa tija na ufanisi mkubwa.
Aidha, amewataka watendaji wote wanaosimamia miradi ya nishati safi ya kupikia na utunzaji wa mazingira wahakikishe wananchi wote wanashirikishwa kikamilifu katika kampeni zote ili nchi ipate matokeo ya haraka.