Mwanamfalme, Prince Dube ametangaza rasmi kuondoka Azam FC akieleza kuwa miaka minne aliyowatumikia matajiri wa Dar es Salaam imebeba historia kubwa kwenye maisha yake ya soka.
“Nikielekea kuanza ukurasa mpya, ninaondoka nikiwa na mafunzo niliyoyapata katika muda wakuwa Azam. Uungwaji mkono niliopata kutoka mashabiki umekuwa mwema na wenye manufaa kwangu na nitaukumbuka na kuutukuza daima,” ameandika Prince Dube.
Katika barua yake aliyoichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram ameeleza kuwa anaamini Azam FC itaendelea kukua na kufanya vizuri, na anawatakia heri na furaha wachezaji, wakufunzi na mashabiki.
Dube ambaye mwishoni mwa wiki aliandika barua kwenda Azam akiwaeleza kuhusu kutaka kuondoka amefuta picha zake akiwa na klabu hiyo katika ukurasa wake wa Instagram, kitendo kinachoashiria uhusiano usio mzuri baina ya pande hizo.
Tangu alipotua Azam Complex mwaka 2020, Dube ambaye amekuwa akiandamwa na majeraha ameichezea Azam michezo 32 akiifungia magoli 34.
Licha ya kuwa raia huyo wa Zimbabwe hajaeleza anakoelekea, baadhi ya mashabiki wamemhusisha na kujiunga na mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga SC.