Kazi ya kuondoa tope kwenye mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Chini lililosababisha kupungua uzalishaji kwa asilimia 20 iko mbioni kukamilika.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Kiula Kingu amesema uchafu kwenye maji umesababisha tope katika machujio ya maji na hivyo kuathiri ubora na usafi wa maji yanayozalishwa kwenda kwa watumiaji.
“Tuliona ni vyema kutenga muda wa saa 36 kusafisha machujio ya maji ili kuwezesha kupatikana kwa maji yaliyo safi na yenye ubora kwa watumiaji. Kazi ya kuondoa tope kwenye chujio kubwa ilianza tangu siku ya Jumanne na inafanyika usiku na mchana,” amesema Kingu.
Amesema kazi imefikia hatua nzuri na itakapokamilika wataruhusu baadhi ya pampu kuwashwa na huduma ya maji kurejea kwenye hali yake.
Amewataka wananchi wanaoharibu miundombinu ya maji hasa kipindi hiki cha mvua kuacha mara moja kwa kuwa uharibifu huo unasababisha gharama kubwa kwa Mamlaka ambayo inalazimika kusafisha mtambo kila mwezi tofauti na awali ambapo mtambo ulikuwa ukisafishwa kila baada ya miezi sita.