Waziri Mkuu wa Peru ajiuzulu

0
228

Waziri Mkuu wa Peru, Alberto Otarola amejiuzulu baada ya tuhuma za kudaiwa kutumia ushawishi ili mpenzi wake apate kandarasi ya biashara na serikali kupitia sauti yake iliyorekodiwa kurushwa kwenye vyombo vya habari.

Hata hivyo, Otarola amekanusha madai hayo akisema ni mkakati uliosukwa na wapinzani wake wa kisiasa.

Aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu jana baada ya kipindi cha televisheni cha Panorama kurusha sauti inayodaiwa kuwa ni yake.

Akitangaza hatua hiyo, Otarola amewaambia waandishi wa habari mjini Lima kuwa sauti hiyo imeandaliwa na wapinzani wake wa kisiasa.

Amedai kuwa wapinzani wake wameibadilisha na kuihariri sauti yake ili kutekeleza matakwa yao na kwamba kimsingi baadhi ya maneno yake ya asili kwenye sauti hiyo aliyasema mwaka 2022 kabla ya kuingia madarakani.

Amesema anajiuzulu ili kumpa rais ‘utulivu’ wa kuunda tena baraza la mawaziri.