Malalamiko 200 yanafika CCM kwa siku

0
437

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda amesema kutokana na changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali nchini kutotatuliwa kwa wakati, chama tawala kimekuwa kikipokea malalamiko yao lukuki kila uchwapo

Akitoa tathmini ya ziara yake ya mikoa 20 nchini kwa waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Makonda amesema wananchi wamekuwa wakipeleka malalamiko yao katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), Makao Makuu Dodoma pamoja na ofisi ndogo ya chama hicho iliyoko Lumumba, Dar es Salaam. Wakati mwingine amesema idadi ya malalamiko inafikia 200 kwa siku.

Amesema watendaji wengi wa Serikali wamekuwa wakipokea malalamiko ya wananchi bila kuyatatua na hivyo kusababisha wananchi kutafuta njia nyingine mbadala ili kupata msaada. Amesema kutokana na watendaji kutotatua kero za wananchi ipasavyo, imepelekea wananchi kuichukia serikali yao na ndio maana wanajitokeza kwenye ofisi na mikutano ya CCM kuomba utatuzi wa kero zao.

“Nawaombe sana watendaji katika Ofisi za Serikali mhakikishe mnatatua changamoto za watu ili kujenga imani ya wananchi kwa chama na Serikali,” ameongeza Makonda.