Kwa mujibu wa taratibu za misiba ya viongozi wa kitaifa, bendera iliyotumika kufunika jeneza lenye mwili wa marehemu aliyekuwa rais mstaafu baada ya mazishi hukabidhiwa kwa familia ya marehemu.
Halikadhalika, mazishi ya kiongozi ambaye msiba wake ni wa kitaifa, misingi na taratibu za dini hufuatwa pamoja na mila na desturi ya marehemu kufuatana na sababu za kifo kama ambavyo Kamati ya Mazishi ya Kitaifa itakavyoona inafaa.
Endapo msiba ni wa rais mstaafu basi siku za maombolezo huwa ni saba na bendera hushushwa nusu mlingoti.
Ili kutoa heshima za mwisho, mwili wa marehemu huwekwa kwenye uwanja wa maombolezo au mahali pengine kama ambavyo Kamati ya Mazishi ya Kitaifa itakavyoona inafaa.
Vilevile muda wa kutoa heshima za mwisho kwa kiongozi wa kitaifa huamuliwa na Kamati ya Mazishi ya Kitaifa kwa kushirikiana na familia ya marehemu au kiongozi wa dini ya marehemu anayehusika.
Mazishi ya kiongozi wa kitaifa huwa na gwaride maalumu lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kwenye eneo la mazishi kwa kushirikiana na Kamati ya Mazishi ya Kitaifa.
Ikiwa mazishi ni ya rais mstaafu, basi mazishi hayo huhusisha gwaride lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) likiwa na gadi moja iliyokamilika (full guard) na kupigwa Wimbo wa Taifa.
Sambamba na hilo, mizinga 21 hupigwa wakati wa mazishi karibu na eneo la makaburi.