Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro ametaja maeneo ambayo mwili wa Hayati Rais Ali Hassan Mwinyi utapita kwa ajili ya kwenda Uwanja wa Uhuru kuagwa.
“Tumejipanga kwa msiba huu, njia ambazo zitatumika zitakuwa mbili; njia ya kwanza ni kutoka Mikocheni tutapitia Shoppers pale Morocco lakini tutakwenda msikitini kwa ajili ya ibada,” amesema Kamanda Muliro.
“Tukitoka kwenye ibada tutarudi kutoka (Barabara ya) Morocco kwenda Magomeni, kwa maana tutapita Manyanya, Mkwajuni hadi Kigogo na tutapita karibu na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
“Baada ya ofisi hiyo, mwili utakwenda hadi Veta mpaka Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (Duce) na kuishia Uwanja wa Uhuru. Hizo ndizo njia tutakazotumia, kwa hiyo wananchi watakaopenda kuwa barabarani watakuwa kwenye njia hizo.”
“Utaratibu mzuri utakuwepo pale uwanjani ndani na nje. Watu wanahimizwa waje kumuaga mpendwa wetu,” amesema Kamanda Muliro.
Mwili wa Rais Mwinyi atakayezikwa kesho Unguja, unaagwa leo ljumaa, Machi Mosi, 2024 jijini Dar es Salaam katika Uwanja wa Uhuru.