Setilaiti kongwe yaangukia Bahari ya Pasifiki

0
4215

Setilaiti ya Ulaya ambayo ilianzisha teknolojia nyingi zinazotumiwa leo katika kufuatilia sayari na hali ya hewa, imeteketea baada ya kuungua ikiwa angani na mabaki yake kuanguka katika Bahari ya Pasifiki.

Hadi asubuhi hii, hakukuwa na mashuhuda wa kuona mabaki ya chombo hicho chenye uzito wa tani mbili katika maeneo mengine ya uso wa dunia.

Sehemu kubwa ya mabaki yake yameangukia Bahari ya Pasifiki Kaskazini, kati ya Alaska na Hawaii, takribani kilomita 2,000 magharibi mwa California.

Setilaiti hiyo, ERS-2, iliyozinduliwa na Shirika la Anga za Juu la Ulaya katika miaka ya 1990 ililenga kuchunguza angahewa, ardhi na bahari kwa njia ambayo wakati huo ilikuwa mpya.

Ilifuatilia hali ya mafuriko, kupima halijoto ya eneo la nchi kavu na bahari, ilifuatilia mienendo ya sehemu za barafu na kuonesha mshindo wa ardhi wakati wa tetemeko la ardhi.

Jana baada ya habari hii kuonekana mitandaoni ikionesha kwamba dude hilo linaweza kuangukia kokote duniani, baadhi ya wasomaji wetu walionesha hofu huku wengine wakiona ni fursa kwamba likiangukia maeneo yao watapata chuma chakavu.