Makatibu Wakuu kutoka wizara Tano za Tanzania na Uganda wanakutana mjini Bukoba mkoani Kagera, kujadili mambo mbalimbali yanayozihusu nchi hizo.
Makatibu hao Wakuu wanatoka wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Maji na wizara ya Nishati.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Dkt Faraja Mnyepe amesema kuwa, mkutano huo ni mfululizo wa mikutano kati ya Tanzania na Uganda yenye lengo la kutatua changamoto zinazozikabili nchi hizo kwa nia ya kuleta maendeleo.
Dkt Faraja Mnyepe amesema kuwa, pamoja na kuwepo kwa changamoto kadhaa, Tanzania na Uganda zinaendelea kufurahia uhusiano mzuri uliodumu kwa muda mrefu.
Kabla ya kuanza kwa mkutano huo wa siku Mbili wa Makatibu Wakuu kutoka wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wizara ya Mifugo na Uvuvi, wizara ya Maji na Wizara ya Nishati kutoka nchi za Tanzania na Uganda, Wataalamu wengine wa wizara hizo kutoka nchi hizo Mbili walikutana na kujadili changamoto mbalimbali, na mapendekezo yao yanawasilishwa katika mkutano huo wa Makatibu Wakuu.
Baadhi ya Changamoto zinazojadiliwa kwenye mkutano huo wa Makatibu Wakuu ni uimarishaji na uthamini wa mpaka wa Kimataifa wa Tanzania na Uganda, mpango wa utunzaji mto Kagera na matumizi endelevu ya rasilimali kati ya Tanzania na Uganda katika Bonde la Mto Kagera.