Kwa nini ninataka wanitoe uhai

0
281

Joe Mudukiza, 28, mkazi wa Nairobi, Kenya aligundulika kuwa na ugonjwa wa seli mundu akiwa na umri wa miaka miwili. Lakini kuanzia mwaka jana ugonjwa huo umekuwa ukimsumbua kijana huyo na kumpa maumivu makali.

Sasa anataka kusaidiwa kiafya ili afe, lakini kila mtu anayemzunguka anapinga uamuzi wake. Ni hatua moja tu iliyobaki kwake kusafiri hadi Ubelgiji kwa ajili ya utaratibu huo anaoutaka!
Akizungumza katika mahojiano, Joe amesema kwa muda wa miezi mitano, akili yake imekuwa na mawazo ya kifo chake tu.

“Hii ni mara ya kwanza, katika miaka 26, ambapo nimechagua kuonesha ulimwengu udhaifu wangu. Nimefanya azimio la kupata amani, ikiwa nitaipata baada ya haya maisha ya dunia,” anasema.

Anaongeza, “Ninachoomba ni cha ajabu kwa watu wangu, utamaduni wangu na sheria za nchi yangu; Je, afadhali niishi na maumivu yasiyovumilika, yanachoma kila seli katika mwili wangu au nipumzike?

“Nakumbuka nikiwa nimezungukwa na wauguzi waliokuwa wakijaribu kutafuta mishipa yangu bila mafanikio, lakini maumivu yalizidi kila dakika. Hilo lilidumu kwa saa sita, na niliporudi nyumbani baada ya hapo, nilianza kutafiti kuhusu watu wanaosaidiwa kufa. Nimetazama video nyingi za YouTube za watu waliochagua kusaidiwa kufa. Nimesoma kila nyenzo zinazoweza kuwa kwenye mtandao kuhusu mauaji ya rehema. Sasa najua baadhi ya sheria pia,” anasema.

Anasema kwa kuwa Kenya sheria haziruhusu kusaidiwa kufa, ameanza mawasiliano na taasisi moja ya Ubelgiji inayosaidia watu wanaotaka kufa ya Association for the Right to Die with Dignity na kwamba wameonesha utayari wa kumsaidia.