Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amewataka wasomi nchini kubadili fikra zao kwa kutumia akili vumbuzi na sio akili kibarua ili kulisaidia taifa kusonga mbele kwa maendeleo.
Dkt. Mollel amesema hayo leo Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, Ameir Abdallah Ameir aliyetaka kujua ni tafiti zipi ambazo taasisi za tiba asili zimekamilisha na kuweza kuwa suluhisho la maradhi mbalimbali kama Tiba Mbadala.
Dkt. Mollel amesema kuwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2024 zaidi ya tafiti 50 zimefanyika ndani ya nchi juu ya ubora na usalama wa dawa zinazotumika kwa tiba asilia kwa kupitia Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).
Ameongeza kuwa baadhi ya tafiti hizo ni pamoja na utafiti wa dawa ya Saratani ya NIMREGENIN, Dawa ya TANGHESHA inayotibu Selimundu, Dawa ya PERVIVIN inayotibu tezi dume, Dawa ya WARBUGISTAT inayotibu magonjwa nyemelezi na Dawa ya NIMRICAF inayotibu Mfumo wa upumuaji.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanatunza miti inayotumika kutengeneza dawa za tiba asili ili kuendelea kuzalisha dawa za tiba asili za kutosha nchini.