Rais John Magufuli amewaahidi wakulima wa wilaya ya Kyela mkoani Mbeya kuwa serikali itaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili wanufaike na kilimo chao.
Rais Magufuli ametoa ahadi hiyo wilayani Kyela wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara na wakazi wa wilaya hiyo.
Amesema kuwa miongoni mwa jitihada kubwa zilizofanywa na serikali kwa lengo la kumsaidia mkulima, ni kuendelea kufufua vyama vya ushirika ambavyo vitamuondoa mkulima katika unyonyaji.
Akizungumza na wakazi hao wa Kyela, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku Nane mkoani Mbeya, Rais Magufuli ametoa wito kwa wakulima wa wilaya hiyo pamoja na mkoa huo kukopa katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo Nchini (TADB) kwa kuwa ipo kwa ajili yao.
Amesema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa, japo mkoa wa Mbeya una idadi kubwa ya Wakulima na ambao wamekua wakifanya vizuri katika kilimo, wamekua hawakopi TADB tofauti na wakulima wa mikoa mingine.
Amewakumbusha Watendaji wote wa halmashauri nchini, kuhakikisha Wakulima hawatozwi tozo za kilimo zilizofutwa, kwani kwa kufanya hivyo ni ukiukwaji wa sheria.