Jikingeni na ugonjwa wa moyo

0
232

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema jitihada zinahitajika katika kutoa elimu ya magonjwa yasiyoambukiza pamoja na kuzingatia mtindo bora wa maisha, mazoezi na kufanya vipimo vya afya mara kwa mara ili kukabiliana na maradhi mbalimbali.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo unaofanyika Zanzibar.

Amesema katika kukabiliana na ugonjwa wa moyo ni muhimu Wananchi wakafuata njia za kujikinga zaidi ikiwemo kuacha ulevi uliopindukia, uvutaji sigara, tabia bwete pamoja na uzito uliopindukia.

Dkt. Mpango ametoa rai kwa Watalaamu wa afya, wasomi, vyombo vya habari na watunga sera kushiriki katika utoaji elimu kuhusu masuala ya afya.

Makamu wa Rais amesema Tanzania imechukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya moyo kama vile kuimarisha Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na kufanya tafiti za afya za kimkakati ili kupata suluhu ya changamoto mbalimbali za kiafya zinazowakabili Wananchi.