Katika Warsha iliyofanyika jijini Nairobi inayohusu kujenga uchumi endelevu katika utunzaji wa mazingira, pamoja na mambo mengine waandishi wa habari kutoka nchi za Mashariki na Mangharibi mwa Afrika walipata fursa ya kujifunza zaidi juu ya umuhimu wa uchumi endelevu katika uhifadhi wa mazingira.
Mada zilizowasilishwa ni pamoja na njia zitakazotumika kutoa suluhisho la kufikia lengo la kuhakikisha taka zinapungua kwenye majalala na mazingira yanayoizunguka jamii kupitia utaratibu wa taka hizo kutumika kutengeneza bidhaa nyingine, kuhuishwa au kurejeshwa katika hali ya upya huku mchakato huo ukiwa na uhakika wakumwingizia mwananchi kipato.
Uchumi endelevu katika uhifadhi wa mazingira umepewa kipaumbele cha kuwa mbadala wa uchumi wa kitamaduni ambao umeelezwa kuwa ulilenga zaidi kutengeneza, kutumia, na kutupa bidhaa pindi zinapokwisha muda wake au kuharibika ambapo lengo kuu ni kuzitunza rasilimali zilizopo ili zitumike kwa matumizi ya muda mrefu iwezekanavyo ili kupunguza ongezeko la taka huku mwananchi akijikwamua kiuchumi kupitia na mchakato huo.
Baadhi ya njia zilizopendekezwa za kufikia uchumi endelevu katika uhifadhi wa mazingira ni kupunguza matumizi ya malighafi mpya katika kutengenza bidhaa mpya kwa kuichukua bidhaa iliyoharibika au chakavu na kuiboresha au kuhuisha bidhaa hiyo ili irudi katika hali yake ya upya kama ilivyokuwa awali.
Watengenezaji wa bidhaa watakiwa kuwa wahusika wa kwanza kuwajibika kulinda mazingira kutokana na uharibifu unaoweza kusababishwa na bidhaa wanazozitengeneza kwa kuweka mazingira yatakayomshawishi mwananchi kurudisha kwake kifaa au bidhaa iliyoharibika au kuchakaa ili aweze kuirudisha katika matumizi au kuichakata kuwa nishati ikiwa haiwezekani tena kuhuishwa.
Bidhaa zinazozalishwa viwandani zatakiwa kuwa na sifa ya kurekebishika au kuhuishwa pale zinapoharibika au kumalizuka matumizi yake huku mazingira ya kuzirekebisha bidhaa chakavu na mbovu yawe ni rafiki yanayofikika kwa wepesi.
Aidha, pendekezo jingine ni kuwa bidhaa chakavu zilizokwisha muda wake au zisizohitajika tena ikiwa haiwezekani kuzihuisha au kutengeneza, zibadilishwe kuwa nishati [energy] itakayotumika kuendesha shughuli mbalimbali badala ya kuzitupa jalalani.
Ukiwa kama mdau wa mazingira, kwenye jamii inayokuzunguka unadhani ni njia zipi nyingine zinaweza kutumika kwa dhana hii ya uchumi endelevu katika uhifadhi wa mazingira?