Dawa za kulevya aina ya Heroin na Methamphemine, kilogramu 3,182, zimekamatwa zikiwa kwenye vifungashio vya kahawa na majani ya chai mkoani Dar es Salaam na mkoani Iringa katika operesheni iliyofanywa na Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kati ya Desemba 5 hadi 23 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Kamishna Jenerali, Aretas Lyimo amesema tangu udhibiti uanze DCEA haijawahi kukamata kiasi kikubwa cha dawa kama ilivyo sasa na iwapo zingeingia sokoni, watu milioni 76.3 wangeathirika.
Amesema kiasi hicho cha dawa kinajumuisha kilogramu 2,180.29 za dawa aina ya Methamphemine na kilogramu 1001.71 aina ya Heroin zilizokamatwa katika wilaya za Kigamboni, Ubungo na Kinondoni kwa Dar es Salaam na mkoani Iringa.
Amesema, katika operesheni hiyo watu saba wamekamatwa kati yao wawili ni raia kutoka bara la Asia.
Aidha, Lyimo amesema mbinu ambayo imekuwa ikitumika kufunga dawa hizo kwenye vifungashio vya bidhaa zenye chapa mbalimbali ikiwemo kahawa na majani ya chai inatumika kwa lengo la kurahisha usafirishaji wake na kukwepa kubainika.
Amesema dawa ya Methamphemine ni dawa mpya ya kulevya iliyopo katika kundi la vichangamshi sawa na Cocaine.