Ubinafsi unakwamisha maendeleo ya Kagera

0
235

Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ameendelea kuwanyooshea kidole baadhi ya viongozi wanaochangia kurudisha nyuma maendeleo ya mkoa wa Kagera na kutoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kusimama kidete kwa umoja kuhakikisha wanabadilisha historia iliyopo katika mkoa.

Ameyasema hayo mjini Bukoba wakati hafla ya Chakula cha jioni ya “Ijuka Omuka” iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa Kagera, Hajjat Fatma Mwassa iliyolenga kuwakutanisha Wanakagera wanaoishi ndani na nje ya nchi na kurleza kuwa “Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa mkoa wa Kagera alituelekeza kufanya hili tunalolifanya leo la kujadili mustakabali wa mkoa wetu,” amesema Bashungwa.

Bashungwa ameeleza kuwa maendeleo ya mkoa wa Kagera yamekuwa yakirudishwa nyuma na baadhi ya viongozi na wanasiasa ambao wamekuwa wakipambania maslahi yao binafsi na kukwamisha maendeleo ya mkoa kwani licha ya Serikali kutoa fedha za miradi mbalimbali bado kumekuwepo na viongozi wanaoendelea kukwamisha utekelezaji huo.

Ameeleza baadhi ya matukio mengine yaliyochangia kudumaza maendeleo ya mkoa kiuchumi, kijamii na kisiasa ni pamoja na vita, milipuko ya magojwa, majanga ya asili kama tetemeko na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Kagera, Fatma Mwassa amesema mkoa huo hauwezi kuendelea bila ushirikiano, kupingana kwa kila jambo, kuwekeana figisu na mikingamo bali mkoa utafanikiwa kwa kuwa na umoja madhubuti.