KUPANDISHA KODI YA POMBE KUTAPUNGUZA VIFO

0
855

Shirika la Afya Duniani (WHO) hivi karibuni limetoa taarifa yenye data mpya inayoonesha namna ongezeko la kodi na ushuru katika pombe linaweza kuchangia kupunguza vifo.

Shirika hilo limebainisha kuwa nchi nyingi duniani hazitumii mchakato wa kukusanya kodi na ushuru kama nyenzo ya kuhamasisha tabia bora za kiafya hivyo shirika hilo limetoa mwongozo wa kiufundi kuhusu sera na usimamizi wa kodi ya pombe.

Kwa mujibu wa taarifa ya WHO watu milioni 2.6 hufa kila mwaka kutokana na unywaji wa pombe huku zaidi ya watu milioni 8 wakipoteza maisha kutokana na lishe isiyofaa hivyo kwa kupandisha ushuru na kodi ya pombe kutasaidia kupunguza vifo hivyo.

Hata hivyo taarifa hiyo imeeleza kuwa divai [wine] haitozwi ushuru katika nchi 22 ambazo zipo ukanda wa ulaya.

Kwa wastani ulimwenguni ushuru wa juu wa pombe unatajwa kuwa takribani 17.2% kwa vinywaji vya bia [beer] na 26.5% kwa pombe kali [spirits].

Tafiti zilizofanywa mwaka 2017 zinaonesha kuwa ikiwa bei ya pombe itaongezwa kwa zaidi ya 50% ingesaidia kupunguza vifo milioni 21 katika kipindi cha miaka 50 huku takribani dola trilioni 17 zikiongezeka kama mapato ya ziada kwa nchi husika.

Aidha taarifa hiyo imeitaja nchi ya Lithuania kama mfano ambapo iliongeza ushuru wa pombe katika mwaka 2017 ili kupunguza unywaji imesaidia kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa yanayohusishwa na unywaji Pombe kutoka vifo 23 katika watu laki moja kwa mwaka 2016 hadi kufikia vifo 18 mwaka 2018.