MIKAKATI YA TANZANIA KUELEKEA MKUTANO WA COP28

0
290

“Afrika ni mama wa mazingira na inalinda mazingira yake.” Haya yamebainishwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki unaoendelea mkoani Arusha unaojadili kwa pamoja masuala ya mabadiliko ya tabianchi na usalama wa chakula katika ukanda huo.

Serikali ya Tanzania imeeleza mikakati yake iliyowekwa pamoja na ile ambayo imeaanza kutekelezwa kuelekea mkutano mkuu wa kimataifa unaojadili masuala ya mazingira (COP28), namna ambavyo Tanzania inakabaliana na hewa ukaa katika jitihada za uhifadhi na utunzaji wa mazingira.

Akitaja mikakati mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira Rais Dkt. Samia amesema katika jitihada za kupunguza hewa ukaa (greenhouse gas emissions) Tanzania imeweka malengo ya kupunguza hewa ukaa kwa asilimia 35 ambapo katika mkakati huo yapo maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya mchakato huo.

Amebainisha kuwa tayari Serikali imetenga hekta milioni 48 ambazo ni sawa na asilimia 55 ya ardhi yote ya Tanzania ambayo ipo chini ya uhifadhi wa mazingira na kuwa uwepo wa maeneo hayo yanaifanya Tanzania kuwa nchi pekee Afrika Mashariki kuwa na eneo kubwa zaidi la kukabiliana na hewa ukaa [carbon sink plant].

Ameikaribisha sekta binasfi kushiriki katika mchakato mzima wa kukabiliana na hewa ukaa akitoa wito kwa sekta hiyo kuleta teknolojia ambayo itasaidia kuotesha misitu mingi zaidi katika maeneo hayo ili kufikia lengo lililotengwa.

Rais Dkt. Samia ameongeza kuwa, ni matarajio kuwa sekta binafsi itafanya biashara ya hewa ukaa na tayari serikali imeweka kanuni mbayo inaipa sekta hiyo mamlaka ya kufanya biashara hiyo.

Sambamba na hilo ameeleza kuwa kwa kutekeleza makubaliano ya Paris [Paris agreement] kuwa serikali zinapaswa kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kushiriki biashara ya hewa ukaa, hivyo tayari Serikali ya Tanzania imeweka kanuni zinazoiruhusu serikali kwa serikali kuingia makubaliano ya kufanya biashara ya hewa ukaa ambapo nako ushiriki wa sekta binafsi unahitajika.

Kuelekea mkutano mkuu wa kimataifa wa mazingira COP28, Rais Dkt. Samia amesema Tanzania inakwenda na programu ya kuonesha fursa za kilimo cha kisasa [smart agriculture] kinachofanyika nchini na pia inakwenda kuzindua programu ya nishati safi ya kupikia ya wanawake wa Kiafrika (The African women clean cooking support program) yenye lengo la kupunguza matumizi ya kuni kupikia.

Rais Dkt. Samia amehimiza nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kusimama na sauti moja inayosema kuwa Afrika ndio mama wa mazingira kwani ipo kwenye nafasi ya kulinda mazingira. Amewaomba marais wenzake kuwa na kauli moja kama jumuiya wanapoelekea katika mkutano huo wa kimataifa COP28.

“Sasa hapa naomba tuwe na kauli moja kama East Africa Block kwamba tunapokwenda kule, na ndio msimamo ambao mawaziri wetu wameweka tunawashukuru kwamba tunakwenda na position [nafasi] moja ya kusema sisi ni mama wa mazingira tunalinda mazingira yetu,” amesema Dkt. Samia.

Akimaliza kuwasilisha mchango wake, ametoa wito kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa pamoja kuweka mikakati, sera na mipango ili kuwa na mwelekeo mmoja katika uwekezaji wa kilimo stahimilivu kwa mazingira na uwekezaji katika nishati jadidifu kuelekea mkutano mkuu wa COP28.