BANDARI NYINGINE KUJENGWA MTWARA

0
310

Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile amesema pamoja na kuwa wizara hiyo ina mipango ya muda mfupi katika usimamizi na matumizi ya bandari ya Mtwara, Serikali inakwenda kujenga bandari nyingine mkoani humo katika eneo linalofahamika kama kisiwa Mgao ambapo kwa sasa hatua za manunuzi zimeanza.

Akizungumza mkoani Mtwara wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa bandari ya Mtwara Naibu Waziri Kihenzile amesema, bandari hiyo mpya itakuwa ni maalumu kwa ajili ya usafirishaji bidhaa zijulikanazo kama ‘bidhaa chafu’ ambazo ni kama makaa ya mawe na saruji.

Amesema wizara ya Uchukuzi inaendelea kuweka mikakati ya namna ya kuimarisha bandari ya Mtwara ili kuhakikisha bidhaa nyingine pia zinasafirishwa kwa wingi.

Katika ziara yake mkoani Mtwara Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile ametembelea na kukagua utendaji kazi wa bandari ya Mtwara na uwanja wa ndege wa Mtwara.