Bashungwa ambana Mkandarasi, atoa siku 14

0
210

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ametoa siku 14 kwa Wakala wa Barabara (TANROADS), Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) na Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB) kuhakikisha mkandarasi aliyepewa kazi ya kujenga barabara ya Ibanda – Kajunjumele – Kiwira/Itungi Port (km 32) analeta vifaa na watalaam wote wanaohitajika eneo la mradi kwa mujibu wa mkataba.

Mradi wa barabara hiyo unafadhiliwa na Serikali kwa asilimia 100 kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 38 ambapo unatekelezwa na mkandarasi kutoka kampuni ya M/s AVM-Dillingham Construction International na kusimamiwa na Kitengo cha TECU kutoka Wakala wa Barabara(TANROADS).

Bashungwa ametoa agizo hilo wilayani Kyela mkoani Mbeya mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo ambayo ipo nyuma ya muda wa mkataba kwa asilimia 25 na kubaini mradi huo una upungufu wa watalaam na vifaa muhimu vinavyohitajika eneo la mradi.

“Naiagiza TANROADS, CRB na ERB kunipa taarifa ndani ya siku hizo na kama mkandarasi akishindwa kutekeleza kama mkataba unavyosema na tutalazimika kuchukua hatua ngumu basi tuzichukue haraka iwezekanavyo”, amesema Bashungwa.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, amesema kuwa mradi huo ni moja ya mikakati ya Serikali ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii mkoani humo kwa kuboresha mtandao wa barabara ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji.

Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri kutoka Kitengo cha TECU, Mhandisi Joel Mwambungu, ameeleza kuwa mkataba wa ujenzi na mkandarasi huyo ulisainiwa tarehe 27 Disemba 2022 na alitakiwa kuanza kazi tarehe 30 Machi 2023 mradi unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 Machi 2025.

Ameongeza kuwa hadi sasa mkandarasi  amefanya maandalizi kwa asilimia 15 tu ukilinganisha na mahitaji ya mkataba na kazi zinazoendelea ni kusafisha eneo la ujenzi ambapo ameshamaliza kilometa 5.