Rais John Magufuli ametoa muda wa wiki moja kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Viwanda na Biashara kukamilisha taratibu za uwekezaji kwa kampuni Sugar Investment Trust (SIT) ya nchini Mauritius ambayo imecheleweshwa kuwekeza katika uzalishaji wa sukari tangu mwaka 2017.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo Ikulu jijini Dar es salaam, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni hiyo Gansam Boodram aliyeongozana na Balozi wa Mauritius nchini Jean Pierre Jhumun.
Katika mazungumzo hayo, Boodram amemweleza Rais Magufuli kuwa yupo tayari kulima ekari Elfu 25 za mashamba ya miwa, kwa ajili ya uzalishaji wa sukari na kwamba uwekezaji huo utawezesha kuzalishwa kwa tani 125,000 za sukari, kutoa ajira za kudumu Elfu Tatu na ajira za muda Elfu Tano, lakini amekwama kutokana na kusubiri majibu kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhusu upatikanaji wa eneo la uzalishaji wa miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari.
Kufuatia maelezo hayo ya Boodram, – Rais Magufuli ameagiza ufanyike uchambuzi wa haraka katika maeneo ya Bonde la mto Rufiji mkoani Pwani, eneo la shamba la Mkulazi mkoani Morogoro na eneo la Kibondo mkoani Kigoma ili mwekezaji huyo apatiwe na kuanza mara moja uwekezaji kwa kuwa nchi inahitaji kuongeza uzalishaji wa sukari utakaomaliza upungufu wa zaidi ya tani Laki Moja ambazo kwa sasa zinaagizwa kutoka nje ya nchi.
Rais Magufuli pia amemuagiza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt Edward Mhede kufuatilia makubaliano ya ushirikiano katika uvuvi kati ya Tanzania na Mauritius ambayo hayajatiwa saini tangu mwaka 2017, licha ya wawekezaji wa Mauritius kuonesha nia ya kutaka kuwekeza katika uvuvi na viwanda vya samaki.
Balozi wa Mauritius nchini Jean Pierre Jhumun naye amemueleza Rais Magufuli kuwa Mauritius ina uzoefu mkubwa katika uvuvi na viwanda vya samaki, na kwamba kwa kuitikia wito wake wa kuhamasisha wawekezaji kuja nchini, amefanikiwa kupata kampuni zilizo tayari kufanya uwekezaji huo baada ya makubaliano kati ya Tanzania na Mauritius kusainiwa.
Rais Magufuli amezionya taasisi za serikali kikiwemo Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) kwa kutoharakisha taratibu za kuwawezesha wawekezaji kuwekeza na amemhakikishia Balozi Jhumun kuwa atafuatilia kuhakikisha uwekezaji wa kampuni ya SIT unafanyika.
“Ndugu zangu watendaji wa Serikali badilikeni, achene kukwamisha wawekezaji, fanyeni maamuzi na kama yanawashinda toeni taarifa kwenye mamlaka za juu”, amesisitiza Rais Magufuli.