Nyongo: Toeni taarifa mkikutana na dawa ambazo si salama

0
315

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Stanslaus Nyongo, ametoa wito kwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba nchini (TMDA) kuendeleza ufanisi wao katika kuchunguza ubora na usalama wa dawa na vifaa tiba ili kulinda afya za Watanzania.

Nyongo alitoa wito huo wakati wa ziara ya kamati yake kwenye Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba kwa lengo la kutathmini shughuli zinazofanywa na mamlaka hiyo katika kulinda afya za Watanzania.

Aidha, Nyongo aliwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa vyombo husika, ikiwa ni pamoja na TMDA kupitia 15200# na kuchagua namba 2, wanapokutana na dawa ambazo si salama na zinaweza kuleta madhara katika jamii. Hii ni ili kushughulikia changamoto hiyo kwa haraka.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, aliwapongeza watumishi wa TMDA kwa juhudi zao kubwa katika utendaji wao unaosaidia kuhakikisha usalama wa wananchi kupitia dawa, vifaa tiba, na vitendanishi.