Watoto 400,000 kupewa chanjo ya Polio Songwe

0
255

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, amebainisha kuwa zaidi ya watoto laki nne wanatarajiwa kupata chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio katika Mkoa wa Songwe.

Waziri Ummy ameyasema hayo wakati akianza ziara yake ya kukagua huduma zinazotolewa katika Halmashauri ya Wilaya ya Songwe ambapo ameanza kutembelea Hospitali ya Wilaya hiyo, Zahanati ya Mbala, pamoja na Kituo cha Afya Mbuyuni kilichopo katika Wilaya hiyo.

“Baada ya kupatikana kwa mtoto mmoja mwenye ugonjwa wa Polio, tumeamua kutoa chanjo ya ugonjwa huo ambapo kwa Mkoa wa Songwe tunatarajia kuchanja watoto takribani laki nne ambao wana umri chini ya miaka nane,” amesema Waziri Ummy.

Amesisitiza kuwa, mwaka 2015 Shirika la Afya Duniani (WHO) liliitangaza Tanzania kuwa ni nchi ambayo imetokomeza ugonjwa wa Polio. Hata hivyo, mwaka huu 2023, Tanzania imepata mtoto mwingine mwenye ugonjwa huo katika Manispaa ya Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa.

Amefafanua kuwa chanjo hiyo itatolewa katika mikoa sita iliyopo mipakani, ambayo ni Mkoa wa Songwe, Kigoma, Rukwa, Katavi, Mbeya, pamoja na Kagera.