JITIHADA ZA SERIKALI KUTAFUTA SOKO LA MAZAO YA TANZANIA

0
189

Rais Samia Suluhu Hassan amekiri kuwepo kwa changamoto ya masoko ya bidhaa zinazozalishwa, lakini Serikali imefanya tafiti na kugundua kuwa kinachopelekea changamoto hizo ni kutofahamu mahitaji halisi ya soko la ndani na nje ya nchi, muunganiko wa soko la bidhaa pamoja na mkulima.

Amesema hayo alipokuwa akijibu swali kutoka kwa kijana aliyehudhuria Mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika 2023 (AGRF) uliofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano Julius Nyerere (JNICC) swali lililohitaji kufahamu ni kwa namna gani Serikali ya Tanzania inatatua changamoto na kuhamasisha upatikanaji wa masoko na uongezaji thamani kwa bidhaa zinazozalishwa na vijana.

Rais Samia amesema katika suala la muunganiko wa soko na mkulima, Serikali imeanza kuweka jitihada hizo kwa baadhi ya mazao kama korosho ambapo imekuwa na matokeo chanya kwa kusaidia kupandisha bei ya korosho kwa kumjengea mkulima ushirika wa moja kwa moja wa soko la bidhaa hiyo kwa kumuondoa mtu wa kati [dalali].

Amesema kwa sasa wanunuzi wananunua korosho kutoka kwenye vyama vya ushirika vya wakulima hivyo wakulima wanapata fursa ya kushindanisha bei, jambo ambalo limepelekea bidhaa hiyo kupanda bei. Rais Samia ameitaja bidhaa ya mbaazi pia ikiwa moja ya bidhaa ambazo zimefanikiwa kupata soko zuri kutokana na jitihada hizo.

Vilevile Rais Samia amesema jitihada zingine Serikali inazochukua ni kuboresha miundombinu ya usafirishaji kwa kujenga barabara zinazounganisha mikoa-mikoa, mikoa -wilaya zake na barabara kuu na nchi za Jirani ili kuyafikia masoko ya nchi jirani kwa kusaidia mazao kutolewa shambani.

Ameongeza kuwa jitihada hizo zinakwenda sambamba na kuboresha bandari zilizopo nchini akiitaja bandari ya Dar es Salaam, Zanzibar, Tanga na Mtwara.

Amesema Serikali inajenga eneo maalumu la kuhifadhi mazao yanayoharibika kwa haraka ili wakati yanasubiri usafiri yaweze kupata hifadhi.

Sambamba na hilo, amesema Serikali imenunua ndege ya mizigo iweze kusafirisha mazao yanayoharibika kwa haraka [Hotculture] kwani ndege hiyo itasafiriaha mazao na kuyapeleka nje jambo ambalo litaepusha kutumia usafiri wa jirani ambao unaweza kuwa na changamoto nyingi ikiwemo za kubadilisha umilika wa bidhaa hizo.

Aidha, Rais Samia amebainisha kuwa Serikali inasaidia kutafuta waongeza thamani kwa mazao ambayo yamepatikana ili yanapoingia sokoni yawe yamekwisha chakatwa.