Kinana : muda wa kusaka uongozi bado.

0
148

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana, ameziagiza kamati za siasa za CCM, kuwafuatilia na kuwachukulia hatua wanachama walioanza kupitapita kusaka ubunge na udiwani.

Amesema wanaofanya hivyo wanakiuka kanuni, utaratibu na miongozo ya uchaguzi ndani ya CCM.

Amesema watakaobainika hawatapitishwa na vikao vya maamuzi kugombea nafasi hizo, hata kama wataongoza katika kura za maoni.

Kinana ameyasema hayo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro katika mkutano mkuu wa jimbo la Hai, uliohusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025, jimboni humo.

“Nataka nitumie fursa hii kuziagiza kamati za siasa za CCM nchi nzima, zikisaidiwa na kamati za maadili nchi nzima, kuwafuatilia wale ambao wameanza kuzungukazunguka kutafuta ubunge, udiwani, uenyekiti wa mtaa au kitongoji kuanzia sasa,” ameagiza Kinana na kuongeza kuwa

“Hatuna nafasi ya kuhangaishwa na watu wanaotafuta uongozi kipindi hiki, wasubiri hadi mwezi wa saba mwaka 2025, Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) itaamua tarehe ya kwenda kuchukua fomu, kabla ya hapo unavunja kanuni”.

Amesema mwana CCM asifikiri kwamba akianza kampeni kabla ya wakati, akapigiwa kura akawa wa kwanza, atapitishwa kugombea.