Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesema Serikali inatambua kuwa mtoto wa kiume yupo katika hatari ya kutopata malezi bora, hivyo ipo katika mchakato wa kuandaa mpango wa malezi na makuzi ya watoto kwenye umri wa awali na mpango wa pili wa kuwawezesha na kuwaendeleza vijana balee kuanzia umri wa miaka 10 hadi 19.
“Tutajikita zaidi katika kuongezea nguvu zaidi tuje na programu za kimkakati zinazojikita zaidi kwenye masuala ya watoto wa kiume, zamani watoto wa kiume walikuwa wanapelekwa jando lakini sasa tutakuwa tunawapeleka jando la kisasa na miongozo yao mizuri mizuri inayosema namna ya kuwa baba wazuri ili watakapo balee wajue changamoto watakazokutana nazo kwenye ndoa kwamba ndoa si mchezo.” Amesema Dkt. Dorothy Gwajima na kuongeza kuwa
“Ni kweli kabisa tunatambua kuwa mtoto wa kiume tofauti na awali anakumbwa na changamoto nyingi sana zitokanazo na mmonyoka wa maadili, anakosa malezi na makuzi bora kiasi kwamba sasa hata akijakuwa baba atashindwa kuwa baba mzuri wa kupambana na changamoto za familia.”
Dkt. Gwajima ameyasema hayo Bungeni, Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa jimbo la Hai, Saashisha Mafuwe ambaye amehoji mpango wa Serikali katika kulinda na kumjengea mtoto wa kiume uwezo.
“Hivi karibuni kumeibuka utamaduni wa kumtetetea mtoto wa kike lakini tunao utamaduni wetu ambao mtoto wa kiume ni baba au kiongozi wa familia. Je, serikali ina mpango gani wa kumjengea uwezo mtoto wa kiume.” amehoji Mbunge Saashisha