ELIMU YA KIKOKOTOO KUENDELEA KUTOLEWA

0
202

Serikali imesema itaendelea kutoa elimu ya kanuni mpya ya mafao ya Pensheni (Kikokotoo) na hadi kufikia Juni 30, 2023 Wanachama wa mifuko ya Pensheni 131,497 na waajiri 5,580 wamefikiwa na elimu hiyo.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Patrobas Katambi amesema hayo bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Moshi Mjini (CCM), Priscus Tarimo aliyetaka kujua mpango wa Serikali kuhusu malalamiko ya wastaafu juu ya Kikokotoo kinachotumika kupiga mahesabu na kulipa mafao.

Aidha, amesema elimu hiyo itaendelea kutolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kushirikiana na Shirikisho la vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).

Naibu Waziri Katambi amesema mpango wa Serikali ni kuendelea kuwaelimisha Wananchi hususani waajiri na wanachama wa mifuko hiyo wakiwemo wastaafu kuhusu faida ya kanuni hizo.