Dkt. Mabula: Tokeni ofisini mkatatue changamoto za ardhi

0
176

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula baada ya kupokea malalamiko kwa wananchi wilayani Ludewa kukosa hatimiliki za ardhi, amewaelekeza
watumishi wa sekta ya ardhi nchini kuhakikisha wanakuwa na kliniki za ardhi ili kutatua changamoto za sekta ya ardhi.

Dkt. Mabula ametoa maelekezo hayo wilayani Ludewa mkoa wa Njombe kufuatia kupokea malalamiko mbalimbali kuhusu changamoto za sekta ya ardhi katika mkutano wa hadhara akiwa katika ziara yake ya siku tatu mkoani Njombe ambayo imeambatana na kukabidhi hatimilki kwa wananchi waliokamilisha taratibu za kupatiwa hati.

Katika mkutano huo, wananchi walimlalamikia waziri Mabula kuwa, wamekuwa wakipata usumbufu kutoka kwa watendaji wa sekta ya ardhi katika mambo mbalimbali yanayohusiana na sekta ya ardhi jambo linalowafanya kushindwa kupata huduma stahiki ikiwemo hati milki.

Kwa mujibu wa Dkt. Mabula, kupitia kliniki za ardhi watumishi wa sekta ya ardhi watatoka ofisini kwenda kwenye kata na kuweka vikao kwa ajili ya kusikiliza hoja, changamoto na kero za sekta ya ardhi kutoka kwa wananchi na wanaposikiliza lazima watoe majibu papo hapo kwa kuwa wao ndiyo wataalamu wa sekta hiyo.

‘’Kwa sababu wakati mwingine changamoto hakuna isipokuwa elimu, mtu haelewi kwa nini amiliki ardhi kwa nyaraka, mtu hajui akitaka kupimiwa aanzie wapi na mwingine amevamiwa katika eneo lake hajui afanye nini,’’ alisema Dkt. Mabula.