ECOWAS Yaidhinisha Niger Kuvamiwa Kijeshi

0
461

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) imeidhinisha kutumwa kwa kikosi cha dharura kinachoundwa na nchi Wanachama wa Jumuiya hiyo kwenda nchini Niger, ili kurejesha utawala wa kikatiba nchini humo.

Hatua hiyo imefikiwa wakati wa mkutano wa Viongozi wa nchi Wanachama wa ECOWAS uliofanyika mjini Abuja nchini Nigeria.

Wiki mbili zilizopita, yalifanyika mapinduzi ya kijeshi nchini Niger ambayo yalimuondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum.

Kwa sasa Jumuiya ya Kimataifa inataka kurejeshwa kwa utawala wa kiraia nchini Niger na Bazoum arejee madarakani na pia inalitaka Jeshi kuachia uongozi.

Kufuatia ECOWAS kuidhinisha Niger ivamiwe kijeshi ili kurejeshaa utawala wa kikatiba, mataifa ya Marekani na Ufaransa yameunga mkono uamuzi huo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken amesema, ECOWAS ina jukumu kubwa la kuhakikisha utawala wa kikatiba unarejeshwa nchini Niger, hivyo nchi hiyo inaunga mkono uvamizi huo.

Kwa upande wa Ufaransa imesema inaendelea na msimamo wake wa kulaani Mapinduzi ya Kijeshi nchini Niger pamoja na kuzuiliwa kwa Rais Mohamed Bazoum na familia yake.

Imetaka ECOWAS kutekeleza uamuzi wake haraka iwezekanavyo, ili kurejeshwa kwa utawala wa Kikatiba nchini Niger.