Kati ya wagonjwa 470 waliopimwa kwenye hospitali mbalimbali nchini katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari mwaka huu hadi hivi sasa, 307 wamekutwa na ugonjwa wa Dengue na wanatoka mikoa ya Dar es salaam na Tanga.
Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ngugulile amesema kuwa ugonjwa huo wa Dengue ulilipotiwa nchini kuanzia mwaka 2010.
Dkt Ngugulile amesisitiza kuwa ugonjwa huo upo nchini na kuwashauri Watanzania kuua mazalia ya mbu na kujinga na mbu wa mchana ili kuepuka kupata ugonjwa huo unaosambazwa na mbu ajulikanaye kama Aedes.
Miongoni mwa dalili za ugonjwa huo ni mgonjwa kupatwa homa kali ya ghafla, maumivu ya kichwa, misuli, kichefuchefu, uchovu wa mwili na kupatwa vipele vidogo vidogo mwilini, dalili zinazofananishwa na malaria.