Walioficha mafuta Mvomero kukiona

0
165

Kamati ya Usalama ya wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro leo Agosti 01, 2023 imefanya ziara ya kushtukiza ya kukagua vituo vya mafuta ya dizeli na petroli.

Katika ziara hiyo Kamati hiyo imebaini baadhi ya Wafanyabiashara wanaficha mafuta na kuuza Kwa madumu, ili kusababisha taharuki ya upungufu wa mafuta na hivyo kupandisha bei kiholela.

Ziara hiyo imefanyika baada kamati hiyo ya Usalama ya wilaya ya Mvomero kupokea malalamiko kutoka kwa Wananchi kuhusu kufungwa kwa vituo vya mafuta tangu jana Julai 31, 2023 katika maeneo mbalimbali wilayani humo hasa Turiani, huku sababu zikielezwa ni uhaba wa mafuta, jambo lililosababisha mafuta kuuzwa kwa vikopo kwa bei ya shilingi Elfu 10 kwa lita moja.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya wilaya ya Mvomero ambaye ni mkuu wa wilaya hiyo Judith Nguli amekemea tabia ya Wafanyabiashara kuficha mafuta na kuongeza kuwa hiyo ni hujuma kwa Serikali.

Wakati wa msako huo vituo vya kuuzia mafuta wilayani Mvomero vimegundulika kuwa na mafuta ya kutosha ambapo mkuu wa wilaya hiyo amesema lazima sheria ichukue mkondo wake kwa waliobainika kuficha mafuta hayo.