Unywaji wa mtori mwingi hauongezi maziwa kwa aliyejifungua

0
308

Dkt. Issa Rashid, Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Wanawake na Uzazi Hospitali ya CCBRT mkoani Dar es Salaam amesema utamaduni wa baadhi ya wanawake waliojifungua kupewa kwa wingi chakula cha aina moja, mfano mtori, hakumsaidii kupata maziwa zaidi kwa ajili ya mtoto.

Badala yake amehimiza wanawake kuhakikisha kuwa wanapata mlo kamili kwa kula kwa kiasi vyakula vyenye protini, wanga, vitamini, ili kutengeneza maziwa ya kutosha na kuepuka kuongezeka uzito kwa kula chakula zaidi ya ambacho mwili unahitaji.

“Haimaanishi ile kumpa mabakuli mengi ya maziwa, ama mabakuli mengi ya mtori, ndio kutamfanya eti maziwa yawe mengi, hapana. Ulaji huo ndio unaosababisha baada ya kujifungua kunakuwa na mfumuko wa mwili kwa sababu anazidisha chakula anachohitaji,” amesema.

Ametoa rai hiyo akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania cha TBC, ambapo leo ni siku ya kwanza ya Wiki ya Unyonyeshaji maziwa ya mama ambayo huadhimishwa kila mwaka lengo kuu likiwa ni kutoa elimu kuhusu umuhimu wa mama kumnyonyesha mtoto.

Aidha, amekemea imani potofu za baadhi ya wanaume kunyonya maziwa ya wake zao kwa madai kuwa yanaondoa mning’inio wa pombe kwani kwa kufanya hivyo wanawadhulumu watoto haki yao ya kupata maziwa ya kutosha ili kuwa na afya bora.

Ameongeza kuwa baadhi ya watoto ambao hawanyonyeshwi vizuri na kwa muda unaotakiwa ambao ni miaka miwili huathiriwa zaidi na maradhi mara kwa mara na huwa na udumavu wa akili. Kwa upande mwingine amesema wanawake waliojifungua na hawanyonyeshi pia wanajiweka katika mazingira ya hatari ya kupata madhara ikiwemo maziwa kumuuma.