Itilima Walalamikia Bei ya Pamba na Uvamizi wa Tembo

0
273

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulrahman Kinana amewaeleza Wananchi wa Itilima mkoani Simiyu jinsi Serikali itakavyotatua changamoto ya bei ndogo ya pamba nchini na uvamizi wa tembo katika makazi ya wananchi.

Kinana ametoa kauli hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kata ya laini A wilayani Itilima, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, uhai wa chama na kusikiliza changamoto za Wananchi.

Kinana ametoa kauli hiyo baada ya kupokea malalamiko ya Wananchi hasusan Wakulima wa pamba kwamba wanatumia gharama kubwa kulima zao hilo, lakini changamoto inayowakabili ni bei ndogo, hivyo walimuomba awasaidie kufikisha kilio chao kwa chama na Serikali upatikane ufumbuzi wa bei ya pamba.

Kinana amesisitiza kwamba ili kuondoa changamoto ya bei ndogo ya pamba, Serikali kuu ijitahidi kutengeneza viwanda vya kutengeneza nyuzi, kuchakata pamba na kutengeneza nguo kusiwe na ulazima wa kupeleka pamba nje ya nchi.

Kuhusu malalamiko ya Wananchi kuvamiwa na tembo ambao wamekuwa wakisababisha Wananchi kupoteza maisha, Kinana amesema amekaa na viongozi wa ngazi mbalimbali wa wilaya, mkoa na maafisa wa uhifadhi wanyamapori kuzungumzia tatizo la Wananchi kuvamiwa na kuuliwa na tembo.

“Tumezungumza kuhusu fidia kwa watu wanaokufa, tumezungumzia mipaka kati ya wananchi na hifadhi, nitakaporudi nitazungumza na Waziri wa TAMISEMI, Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na Waziri wa Ardhi ili jambo hili lifanyiwe kazi,” Amesema Kinana.