NDC itatue matatizo ya kimataifa

0
234

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amekitaka Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kilichopo Kunduchi, Dar es Salaam kujikita kwenye kutatua changamoto zinazoitikisa dunia kwa sasa na kuwa chachu ya mabadiliko chanya duniani.

Dkt. Mpango ameyasema hayo katika hotuba yake mara baada ya kuwatunuku tuzo ya kifahari, stashahada na shahada wahitimu wa NDC katika mahafali ya 11 ya chuo hicho.

“Napenda kupendekeza kwamba kati ya mambo mengi uzito uwekwe kwenye tafiti zenye kutatua changamoto na kuleta majibu, ili kuweza kupambana na majanga ya kimataifa hasa yale yanayohusiana na ‘radicalization’, ukosefu wa ajira kwa vijana, uhalifu wa mtandao, vita vya kiuchumi, shughuli za kigaidi, dawa za kulevya na usafirishaji wa binadamu, mtiririko wa fedha haramu na mabadiliko ya hali ya hewa,” Amesema Dkt. Mpango.

Ameongeza kuwa NDC ni chuo chenye kukuza na kuimarisha uhusiano wa Tanzania na nchi nyingine, kimataifa na kikanda, hivyo msisitizo ni kwa chuo hicho kuendelea kuinua viwango vyake kimataifa.

“Ikumbukwe pia kuwa wahitimu wa NDC wana uwezo wa kuhudumu kama Mabalozi wa kipekee wa Tanzania katika sekta ya utalii, utamaduni, lugha ya Kiswahili na rekodi ya nchi yetu ya kudumisha amani na utulivu wa kijamii na kisiasa tangu uhuru mwaka 1961. Aidha, Chuo cha Taifa cha Ulinzi kinapaswa pia kutamani kuwa kitovu cha elimu ya usalama na masomo ya kimkakati katika kanda,” Ameongeza Makamu wa Rais.