Mgunda ateuliwa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi Simba SC

0
351

Aliyekuwa Kocha Msaidizi wa Simba SC, Juma Mgunda ameteuliwa kuwa mkurugenzi wa ufundi ambaye atahusika na timu ya vijana chini ya miaka 17 na miaka 20, timu ya wanawake na timu ya wakubwa.

Mgunda alijiunga Simba SC katikati ya msimu uliopita akitokea Coastal Union kama kocha wa muda baada ya miamba hao wa Dar es Salaam kuachana na aliyekuwa kocha wake, Zoran Manojlovic.

Mwalimu huyo amesema kuwa wamezunguka nchi nzima kwa ajili ya programu ya kutafuta vipaji kwa vijana.

Amesema kuwa yeye ni muumini wa kuzalisha vipaji na kwamba ukipita katika timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu ya NBC huwezi kukosa vijana aliowafundisha wakati akiwa Coastal Union.

“Hata mimi wakati nacheza, nilicheza nikiwa kijana, uzee umenikuta kwenye mpira,” amesema Mgunda akisema kwamba baada ya Simba kutoa taarifa sasa watu watajua alipo.

Amesema kabla ya taarifa kutolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula tetesi zilikuwa nyingi mtaani lakini alikaa kimya kwa sababu klabu hiyo ina utaratibu wake wa kutoa taarifa.