Chama cha Waagizaji na Wasambazaji wa Mafuta Tanzania (TAOMAC) kimesema kuwa wanachama wake wanaendelea kuagiza mafuta, na wataendelea kufanya hivyo ili kuhakikisha nchi haikosi mafuta.
TAOMAC imesema hayo katika taarifa yake na kuongeza kuwa licha ya kuwa kwa sasa sekta ya uagizaji na usambazaji wa mafuta inapitia changamoto ya ukosefu wa dola, lakini tayari imekaa vikao na mamlaka zinazohusika, na tayari imeahidiwa kuwa tatizo hilo linatafutiwa ufumbuzi.
Aidha, mamlaka hiyo imekanusha taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinazodai kuwa imekaa kikao na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na kuishia kwenye mtafaruku pamoja na kutokukubaliana.
Imesisitiza kuwa haijakaa kikao na EWURA kwa zaidi ya wiki mbili, na pia haijawahi kuwa na mtafaruku na mamlaka hiyo.