Miezi mitatu yatolewa kukamilisha mradi wa maji

0
281

Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Maji Mhandisi Cyprian Luhemeja ametoa muda wa miezi mitatu kwa kampuni ya Unik Construction Engineering ( UNIK) kukamilisha mradi wa maji wa Mugango – Kiabakari hadi Butiama.

Mhandisi Luhemeja ametoa muda huo mkoani Mara alipotembelea eneo la mradi katika kituo cha Kiabakari na kutoridhishwa na hatua za maendeleo ya utekelezaji wake.

“Kama Serikali tunasema sasa basi, mkandarasi inabidi kukamilisha mradi huu ifikapo tarehe 30 Septemba, 2023 Ili Wananchi wa Mugango- Kiabakari – Butiama waweze kupata majisafi na salama,” amesema Mhandisi Luhemeja

Amesema pamoja na kazi kubwa na nzuri iliyofanyika katika mradi huo, suala la muda halivumiliki tena na ikitokea mkandarasi akishindwa kukamilisha hatua za Kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Kwa upande wake msimamizi wa mradi huo Mhandisi Mashaka Sita amesema, watahakikisha wanamsimamia mkandarasi ili mradi huo ukamilike na Wananchi wapate huduma ya maji.

Mradi wa maji Mugango – Kiabakari – Butiama unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 70 unahusisha ujenzi wa matenki matano, vituo vya kusukuma maji vitatu, vituo vya kuchota maji 48, mtambo wa kuzalisha maji lita Milioni 35 kwa siku pamoja na vituo viwili vya kusukuma maji.