Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali inapoteza mapato makubwa kutokana na kuwepo kwa uwezo mdogo wa uendeshwaji wa bandari ya Dar es Salaam ikiwemo kutumia muda mrefu kupakia shehena, meli kusubiri muda mrefu nangani na bandari kushindwa kupokea meli kubwa.
“Bandari za nchi za jirani zina uwezo wa kubeba meli zenye uwezo wa kubeba makasha 4,000 sisi meli zinazokuja hapa zinabeba makasha 2,400 mpaka 2800 tu. Kama bandari ya Dar es Salaam inataka kuhudumia meli yenye uwezo wa kuhudumia makasha 4,000 kama bandari za nchi za jirani tunahitaji meli hiyo ihudumiwe kati ya siku 10 mpaka siku 13”
“kutokana na uwezo huu mdogo wa kiutendaji wa bandari yetu ya Dar es Salaam ni kuikosesha Serikali mapato makubwa ambayo yangeweza kusaidia katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo inaendelea kutekelezwa hapa nchini”.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam wakati wa mkutano wa wizara hiyo na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kuhusu uwekezaji katika bandari ya Dar es Salaam.