DP World ina uwezo mkubwa duniani

0
181

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali iliamua kuanzisha majadiliano na kampuni ya DP World kutokana na kampuni hiyo kuwa na uwezo na uzoefu mkubwa katika kuendesha shughuli za bandari duniani ukilinganisha na kampuni zingine zilizotuma mapendekezo ya kupata haki ya kuendesha bandari ya Dar es Salaam.

Profesa Mbarawa ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam wakati wa mkutano wa wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kuhusu uwekezaji wa bandari ya Dar es Salaam.

“Lengo kuu la Serikali ni kufungua masoko ya kimkakati katika eneo la bidhaa na biashara ya usafirishaji ndani ya nchi na kanda zinazotuzunguka. Baada ya kufanya mawasilisho ya wawekezaji hao pamoja na kupitia sifa zao za kimataifa na kufanya uchambuzi wa kina.. Serikali iliamua kuanzisha majadiliano na kampuni ya DP World”. Amesema Profesa Mbarawa

Ametaja sababu zilizoifanya Serikali kuamua kuanzisha majadiliano na kampuni hiyo ya DP World ambazo ni;

  1. DP World ina uwezo katika uendeshaji wa shughuli za bandari Barani Afrika, Asia, Ulaya, Marekani ya Kaskazini, Kusini na Australia.
  2. DP World ina uwezo na utaalamu wa kuchagiza mnyororo mzima wa usafirishaji kutoka maeneo ambayo bidhaa zinatoka mpaka kwa walaji wa bidhaa hizo.
  3. DP World inamiliki zaidi ya meli 400 za mizigo kupitia kampuni yake ya P&O Shipping Line, jambo linaloongeza ufanisi katika usafirishaji wa mizigo.