BIL 208 KUJENGA SEKONDARI MPYA NCHINI

0
122

Serikali imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 208 ili zitumike kujenga shule mpya za sekondari kwenye halmashauri zote nchini ikiwa ni maandalizi ya kupokea Wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2024.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Deogratius Ndejembi alipopewa nafasi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa awasalimie Wananchi na watumishi wa halmashauri ya Mtwara Vijijini kwenye kijiji cha Mkunwa, wilayani Mtwara.

“Halmashauri zote nchini, ziko 184 zimepatiwa kati ya sh. milioni 570 na milioni 600 za ujenzi wa shule mpya za sekondari. Tumewapa Wakurugenzi hadi Novemba, mwaka huu wawe wamekamilisha ujenzi huo ili waweze kupokea Wanafunzi ifikapo Januari, 2024.”

Akizungumza na Wananchi hao na watumishi mara baada ya kuweka jiwe la msingi, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali inatambua kuwa halmashauri hiyo ni changa na ndio maana inapeleka fedha ili kuwawezesha watumishi hao watimize majukumu yao.

Ameutaka Wakala wa Majengo nchini (TBA) ambao ni wakandarasi wa mradi huo, wakamilishe majengo kwa haraka ili Wananchi waanze kupata huduma.

“Wananchi wanataraji kuona haya majengo yakikamilika. Kwa hiyo tumieni mbinu ya kujenga usiku na mchana ili yakamilike mapema,” amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa

Amewataka mkuu wa wilaya ya Mtwara na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, wakae na TBA na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ili waandae mradi wa kujenga nyumba za watumishi.