Msimu mpya wa soka 2023/24 utaanza kwa namna yake ambapo utashuhudia wachezaji mbalimbali wakicheza dhidi ya timu za zamani baada ya kusajiliwa katika timu mpya.
Michezo ya Ngao ya Jamii ikitarajiwa kuanza Agosti 9 mwaka huu mkoani Tanga, katika mashindano hayo utashuhudia Feisal Salum (Fei Toto) akishuka dimbani akiwa na Azam FC dhidi ya waajiri wake wa zamani, Young Africans SC kwenye mchezo wa kwanza.
Aidha, katika mchezo wa pili wa Agosti 10, utashuhudia Joash Onyango akiwa na Singida Fountain Gate FC akishuka dimbani dhidi ya waajiri wake wa zamani, Simba SC.
Fei amesajiliwa Azam baada ya kuwepo mvutano wa muda mrefu na Yanga uliopelekea kuwa nje ya uwanja, hivyo watu wengi wanatamani kumuona tena akiwa uwanjani.
Wakati huo huo, wengi wanasubiri kuona Onyango kama ataweza kuwazuia washambuliaji wa Simba, baada ya kuondoka kwa kile kinachodaiwa ni kuchoshwa na lawama ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake kutokana na makosa uwanjani.
Kwa mara ya kwanza bingwa wa Ngao ya Jamii atapatikana baada ya michezo minne, inayohusisha timu nne za juu, tofauti na awali ambapo bingwa alipatikana kwa mchezo mmoja uliohusisha timu mbili zilizoshika nafasi ya juu kwenye msimu uliopita.