Serengeti Boys yawahakikishia Watanzania ushindi

0
281

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametembelea kambi ya timu ya Taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 – Serengeti Boys iliyopo katika jiji la Kigali nchini Rwanda na kuwaeleza kuwa Watanzania wana matumaini makubwa kwao, hivyo waongeze bidii.

Waziri Mkuu Majaliwa alikua nchini Rwanda  kumwakilisha Rais John Magufuli kwenye kumbukumbu ya miaka 25 ya mauaji ya Kimbari.

 Akizungumza na wachezaji pamoja na viongozi wa timu hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa amewataka wahakikishe wanafanya mazoezi ya kutosha ili waweze kushinda mechi zinazofuata.

 “Watanzania wana matumaini makubwa kwenu, nasi tunazidi kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu muweze kuibuka na ushindi katika michezo yenu iliyobaki itakayowawezesha kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia”,amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Waziri Mkuu pia ameipongeza Serengeti Boys kwa namna inavyoitangaza nchi kimataifa kupitia kwenye mashindano mbalimbali wanayoshiriki na kuibuka na ushindi na kwamba endapo itaibuka na ushindi katika michezo yake miwili itakuwa imekata tiketi ya kushiriki mashindano ya dunia nchini Brazil.

Wachezaji hao wamemuahidi Waziri Mkuu Majaliwa na Watanzania wote  kuwa watajitahidi kadiri ya uwezo wao kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mechi zilizobaki ili waweze kushiriki Kombe la Dunia.

Akiwa kambini hapo, wachezaji pamoja na viongozi wa Serengeti Boys wamemkabidhi Waziri Mkuu Majaliwa Kikombe walichokipata baada ya kuichapa timu ya Rwanda katika mashindano maalumu kwa ajili ya kujiandaa na AFCON-U17.

Mashindano hayo maalumu yalishirikisha timu za vijana walio na umri wa chini ya miaka 17 kutoka nchi za Tanzania, Cameroon na Rwanda ambapo Serengeti Boys ilishinda mabao mawili kwa moja dhidi ya Cameroon na kutoka sare ya mabao matatu kwa matatu na Rwanda.